AVDelta News
Skip to main content Skip to page footer

Ndovu maarufu Craig aaga dunia akiwa na umri wa miaka 54

Mbali na pembe zake kubwa, Craig alisifiwa kwa tabia yake ya upole na utulivu wa kipekee. 

Mbuga ya Kitaifa ya Amboseli na dunia kwa ujumla zimepoteza ndovu wa kipekee na maarufu, Craig, aliyefahamika kwa pembe zake kubwa sana zilizogusa ardhi na tabia yake ya utulivu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS), Craig alikufa mapema asubuhi ya Jumamosi akiwa na umri wa miaka 54.

Craig alizaliwa Januari 1972 na mama yake aliyekuwa ndovu mashuhuri, Cassandra, wa familia ya CB.

Aliishi maisha marefu ambayo ni ndovu wachache sana huweza kuyaishi.

"Alikuwa miongoni mwa “super tuskers” wa mwisho barani Afrika – ndovu dume wachache sana ambao kila pembe yao ina uzito wa zaidi ya kilo 45," ikasema taarifa ya KWS.

Leo hii, ni ndovu wachache sana waliobaki wenye sifa hizo, jambo lililomfanya Craig kuwa ishara hai ya urithi wa asili wa Afrika.

Mbali na pembe zake kubwa, Craig alisifiwa kwa tabia yake ya upole na utulivu wa kipekee. Mara nyingi alionekana akisimama kwa subira huku watalii wakimpiga picha na video, kana kwamba alielewa nafasi yake maalum duniani.

“Craig alikuwa balozi wa kweli wa Amboseli na mfano wa mafanikio ya uhifadhi wa wanyamapori,” ilisema KWS.

Craig alizaa ndama kadhaa, kuhakikisha kuwa ukoo wake na sifa zake nzuri zinaendelea kuonekana kwa vizazi vijavyo.

Mwaka 2021, Craig alichukuliwa rasmi kama ishara ya chapa ya Tusker kupitia Kampuni ya East African Breweries Limited (EABL), hatua iliyoonyesha umaarufu wake duniani.

KWS ilisema maisha marefu ya Craig yaliwezekana kutokana na ulinzi wa muda mrefu, mapambano dhidi ya ujangili, ufuatiliaji wa karibu, ulinzi wa mazingira na ushirikiano na jamii za wenyeji.

“Craig aliishi kwa uhuru na usalama, akionyesha kile kinachoweza kupatikana pale wadau wanapoungana kulinda wanyamapori,” iliongeza KWS.

Kifo chake kinaacha pengo kubwa katika juhudi za uhifadhi, huku kumbukumbu zake zikiendelea kuishi kama alama ya matumaini na dhamira ya kulinda urithi wa asili wa Kenya.

Ndovu Craig
Ndovu Craig aliyekufa Januari 3, 2026, akiwa na umri wa miaka 54. Picha/KWS