Tahmeed yasifu dereva wake kuokoa abiria wengi wakati wa ajali
- Created by Juma Namlola
- Habari
Tahmeed pia ilitoa rambirambi kwa familia na marafiki wa abiria waliofariki huku ikitoa pole kwa majeruhi.
Kampuni ya mabasi ya Tahmeed imefafanua kuwa basi lake halikuhusika moja kwa moja kwenye ajali iliyotokea eneo la Konza, Ijumaa usiku.
Badala yake Tahmeed imeusifu ujasiri wa dereva wake aliyejitahidi kudhibiti gari baada ya matatu kugongana na lori na kuingia kwenye mkondo wake.
“Kutokaba na kugongana matatu ya Naekana na lori, matatu ilisukumwa kwenye njia ya basi letu. Dereva wetu alijitahidi kudhibiti gari na kuokoa abiria wote waliokuwa ndani ya basi,” ilisema taarifa ya Tahmeed.
Taarifa hiyo iliongeza: “Tulifanikisha kuwaondoa abiria wote salama na kuwahamishia kwenye basi la uokoaji ili waendelee na safari yao."
Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Mukaa, Hussein Abduba, alisema watu sita walifariki papo hapo.
Abiria wengine saba waliopata majeraha makubwa walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Machakos.
Tahmeed alisema ililazimika kutoa taarifa hiyo ili kuonyesha mazuri yakiyojiri wakati wa ajali hiyo.
"Tunatambua umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na tutaendelea kushirikiana kikamilifu na mamlaka husika ili ukweli wa ajali hii ubainike," ikasema taarifa hiyo.
Tahmeed pia ilitoa rambirambi kwa familia na marafiki wa abiria waliofariki huku ikitoa pole kwa majeruhi waliokuwa wakiendelea kupokea matibabu.
“Mawazo yetu na sala ziko pamoja na walioathirika, tunawatakia majeruhi uponyaji wa haraka,” iliongeza taarifa hiyo.
Uchunguzi wa ajali unaendelea huku mamlaka za usalama barabarani zikitoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria na tahadhari barabarani, hasa kwenye barabara kuu zenye mwendo kasi kama Mombasa–Nairobi.