AVDelta News
Skip to main content Skip to page footer

Tundu Lissu avunja rekodi ya mfungwa wa kisiasa Tanzania

Bw Lissu, ambaye alizaliwa Januari 20,1968, ametimiza umri wa miaka 58, huku akiwa amefikisha zaidi ya miezi tisa akiwa kizuizini.

DAR ES SALAAM, Tanzania

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, Jumanne aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa akiwa bado anazuiliwa katika Gereza la Ukonga.

Bw Lissu, ambaye alizaliwa Januari 20,1968, ametimiza umri wa miaka 58, huku akiwa amefikisha zaidi ya miezi tisa akiwa kizuizini, hali inayomfanya avunje rekodi ya kuwa kiongozi wa upinzani aliyezuiliwa kwa muda mrefu zaidi tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mwaka 1992.

Bw Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, mkoani Ruvuma na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kufuatia kampeni za kisiasa za CHADEMA zilizokuwa zikihamasisha madai ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi chini ya kaulimbiu ya “No reforms, no election”.

Baada ya kukamatwa, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako alisomewa mashtaka ya uhaini pamoja na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria za Tanzania hayana dhamana.

Tangu wakati huo, amekuwa akizuiliwa rumande akisubiri hatua zaidi za kisheria.

Maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa yameibua wimbi la pongezi na jumbe za mshikamano kutoka kwa wanaharakati, wanasiasa na Watanzania mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu Maria Sarungi alimtakia heri ya kuzaliwa kwa maneno mazito.

Amesema Lissu ni kiongozi aliyekubali jukumu gumu kwa niaba ya taifa bila kulalamika, na kwamba muda wake wa kuona matunda ya mapambano hayo unakaribia.

Viongozi wengine wa CHADEMA na wanaharakati wa demokrasia pia walitumia mitandao ya kijamii kusisitiza kuwa kuzuiliwa kwa Lissu hakutazima sauti ya upinzani.

Wamemtaja kama ishara ya ujasiri na msimamo thabiti wa kisiasa nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa na mashirika ya haki za binadamu, muda aliokaa Lissu rumande umevuka ule wa viongozi wengi wa upinzani waliowahi kuzuiliwa tangu miaka ya 1990.

Hali hiyo imeochochea mjadala mpana kuhusu uhuru wa kisiasa, haki za binadamu na matumizi ya sheria za usalama wa taifa.

Hadi sasa, mamlaka za serikali bado hazijatoa kauli mpya kuhusu hatma ya kesi hiyo, huku wafuasi wa Be Lissu na mashirika ya kiraia wakiendelea kutoa wito wa kuachiliwa kwake au kuharakishwa kwa mchakato wa haki.

Tundu Lissu
Tundu Lissu avunja rekodi ya mfungwa wa kisiasa Tanzania. Picha/Hisani