Diwani ya 'Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine' yaingia fainali ya Safal Kiswahili Prize for African Literature
Bw Nuhu Zuberi Bakari (kati) akiwa na wanajopo wengine wakati wa uteuzi wa kutangaza miswada iliyoingia fainali. Picha/Hisani ya Safal
Mswada wa diwani ya ‘Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine’ ulioandikwa na Mkenya Edwin Omindo umeorodheshwa miongoni mwa kazi bora zilizoingia fainali ya Safal Kiswahili Prize for African Literature kwa mwaka 2024.
Tuzo hiyo inadhaminiwa na The Safal Group kupitia kampuni ya Mabati Rolling Mills (MRM), na ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt Lizzy Attere na Prof Mukoma wa Ngugi kwa lengo la kuenzi uandishi katika lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka, kati ya, na kwenda kwenye lugha hizo.
Kwa mwaka huu, miswada 210 iliwasilishwa na kufanyiwa mapitio na jopo la majaji kabla ya kuchaguliwa kwa walioteuliwa kuingia fainali.
Miongoni mwa miswada iliyoingia fainali ni:
Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine – Edwin Omindo (Kenya)
Nderemo za Mtaa – Joel Hamisi (Tanzania)
Kitanzi cha Mauti – Mayassa Abdallah Chembea (Tanzania)
Nyaraka za Wafu – Ali Othman Masoud (Tanzania)
Waadhi – Mohamed Hamid Haji (Tanzania)
Bure Ghali – Bashiru Abdallah (Tanzania)
Laana ya Uovu – Mohamed Idrisa (Tanzania)
Mwalimu Abdilatif Abdalla, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa tuzo hiyo, alisema, “Inafurahisha sana kuona kuwa tangu mashindano yaanze mwaka 2015, Safal Prize imeendelea kuvutia idadi kubwa ya washiriki kutoka nchi mbalimbali. Ubora wa miswada pia umeongezeka kila mwaka, jambo ambalo linaendelea kuitajirisha fasihi ya Kiswahili.”
Washindi wa fainali watatangazwa katika hafla rasmi ya tuzo hiyo itakayofanyika Julai 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Jumla ya dola 15,000 za Kimarekani zitatolewa kwa miswada bora ambayo haijachapishwa katika vitengo vya riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia, na riwaya za picha (graphic novels).
Miswada inayoshinda huchapishwa na Mkuki na Nyota Publishers wa Tanzania, huku mshindi wa ushairi akitafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
Kwa mujibu wa Anthony Ng’ang’a, mmoja wa wadhamini wa Safal Kiswahili Prize:
“Tuzo hii ni zaidi ya kutambua vipaji vya fasihi – ni alama ya kuendeleza utambulisho wa Mwafrika. Kwa kuunga mkono kazi asilia katika Kiswahili, tunalinda na kuinua lugha inayowaunganisha, kuwahamasisha na kuwawezesha mamilioni ya watu barani Afrika.”