Kazi: Vijana walioasi mihadarati walia kubaguliwa
Mwanamume apokea methadone kumsaidia kujinasua kutoka kwa uraibu wa mihadarati. Picha/AVDelta News
Afisa Msimamizi wa Waraibu na Matibabu katika Kituo cha Methadone cha King Fahd, Bw Juma Mwamvyoga. Picha/AVDelta News
Vijana waliojinasua kutoka kwa uraibu wa mihadarati kisiwani Lamu wanaililia serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kuwapa kazi.
Vijana hao walidai kuwa kwa sasa wamebadilika kabisa, hasa kimkondo wa maisha na kwamba ni vyema ikiwa wataaminiwa na kupewa ajira.
Tena kilio chao ni kuwa kutokana na tabia chwara walizotambulika kuwa nazo, waajiri wengi - ikiwemo serikali ya kitaifa, kaunti na hata wanajamii wenyewe, wamekuwa wakiwabagua na kuwasuta.
Hii ni licha ya wao kuasi tabia mbaya.
Wakiongozwa na msemaji wao, Bw Shee Babli, ‘mateja’ hao wa zamani walishukuru mpango uliozinduliwa na serikali ya kaunti ya Lamu wa kuwapokeza matibabu waraibu hao wa mihadarati kupitia unywaji wa dawa aina ya methadone.
Vituo viwili vya methadone vimefunguliwa Lamu ambapo kufikia sasa tayari zaidi ya waraibu 400 wamefaulu kujinasua kutoka kwa janga hilo la mihadarati, hasa matumizi ya kokeni na heroni. Vituo hivyo ni King Fahd kisiwani Lamu na kile cha hospitali ya kisiwa cha Faza.
Bw Babli alisema licha ya kuweza kupokea mafunzo, kutibiwa kupitia methadone na kubadili maisha yao, tatizo kubwa linalowakumba wale wanaopona ni ukosefu wa ajira.
“Waajiri wengi bado wanatuona sisi kuwa wale wale mateja wa zamani, hivyo huwa hawataki ama tuwakaribie au kuwaomba kazi. Ni muhimu wafahamu Bw Babli wa sasa si yule wa miaka mitano iliyopita. Wengi wetu kwa sasa tumebadilika na msitubague. Sisi tumekuwa raia wema. Tupeni hizo ajira na tutatunza majukumu yetu vyema,” akasema Bw Babli.
Bw Athman Khamis, ambaye alikuwa mraibu wa mihadarati kwa zaidi ya miaka 10 na kisha kufaulu kujiokoa kutoka kwa janga hilo, alisema ukosefu wa ajira huenda ukawasukuma kurejelea maisha yao mabaya waliyoyapungia mkono wa kwaheri.
Alisema tayari ameshuhudia baadhi vya marafiki wake waliokuwa wameacha dawa za kulevya wakirudi kwenye uraibu kufuatia msongo wa mawazo uliosababishwa na wao kukosa ajira ili kujikimu kimaisha.
“Huku kuzurura ovyo mitaani kwa kukosa ajira ni kitu kibaya. Kumewasukuma wengi ambao walikuwa wameacha mihadarati kurejelea maisha hayo mabovu. Kaunti na serikali kuu ituonee imani. Watuamini na kutupa hizo ajira hata kama ni zile za kufagia mitaani ili tujukumike,” akasema Bw Athman.
Kauli ya vijana hao iliungwa mkono na Afisa Msimamizi wa Waraibu na Matibabu katika Kituo cha Methadone cha King Fahd, Bw Juma Mwamvyoga, aliyesema karibu asilimia 45 ya wale wanaopokea matibabu ya methadone wanaweza kuaminika, kupewa majukumu na kuyatekeleza vyema.
Bw Mwamvyoga alisema idara yake imesajili jumla ya waraibu wa mihadarati 712 kisiwani Lamu, ambapo wale ambao wamekuwa na bidii ya kupokea ushauri na kutumia methadone mfululizo tena inavyotakikana ni karibu 400.
“Ombi langu kwa serikali, wadau na mashirika ni kwamba ipo haja kuwaamini hawa vijana wanaopona kutoka kwa uraibu wa dawa za kulevya. Niko na karibu vijana 400 wanaotumia vyema methadone na wameonyesha kabisa mwelekeo bora wa maisha yao kubadilika kwa uzuri,” akasema Bw Mwamvyoga.