Buriani Mary Sinaida: Mwanzilishi wa Jerusaleum of Christ Church azikwa Kawangware
Dorcus Mary Sinaida Akatsa alizikwa mtaani Kawangware. Picha/Sancia Kagoni
Mwanzilishi wa Kanisa la Jerusaleum of Christ Church ‘Nabii’ Dorcus Mary Sinaida Akatsa alizikwa mtaani Kawangware mnamo Jumamosi.
Akatsa alipata heshima ya mwisho kutoka kwa waumini wake na wanasiasa mbalimbali ambao walihudhuria.
Waumini ambao walitajwa kuwa walipata nafasi za kazi katika idara ya kutoa huduma za usalama, walimpa heshima ya mwisho kwa kupiga gwaride na kumpigia saluti.
Miongoni mwa maafisa hao ni Veronica Marachi ambaye alimshukuru kiongozi huyo ambaye aliwezesha familia yake kupata makao mapya eneo la magharibi mwa Kenya.
“Asante kwa Mami. Alitununulia shamaba wakati wazazi wangu walikuwa wakichekwa na majirani. Hivi sasa ninayo kazi kutokana na maombi yake,” alikamilisha Bi Marachi.
Kwenye mazishi hayo, wanasiasa kutoka mrengo wa ODM walifika kufariji waumini na familia.
Viongozi hao wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Abdullswamad Sheriff Nassir, seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Seneta wa Vihiga Godfrey Ososti.
Viongozi hao walitaja kuwa kuzikwa kwa mwili wa marehemu katika shamba hilo liliko mtaani Kawangware ni kulinda shamba hilo ambalo pia lilikuwa likimezewa na watu fulani.
Seneta Sifuna alisema atazidi kuungana na wana wa Akatsa--David Jogoo na Moses Sangolo--kuhakikisha mali yake hainyakuliwi.
Alidokeza kuwa alikutana na nabii huyo kabla ya kuchanguliwa kuwa Seneta wa Nairobi huku akiwa naye ataweza kupambana na wanyakuzi hao.
“Alinitembelea kwenye afisi yangu akaniombea na kunielezea matatizo yake. Alihakikisha tiketi yangu ya ndege ya kusafiri kutoka Nairobi hadi Kakamega inapatika kila wakati. Hadi pale nilifanikiwa kuweka mambo sawa,” alisema Bw Sifuna.
Kiongozi huyo aliwataka waumini kutafuta kiongozi mwingine ambaye atavalia kiatu cha nabii huyo ili kuunganisha waumini hao.
“Mungu amechukua yule amekuwa akifikisha dua zetu za maombi kwa Mungu. Hivi sasa tunaomba Mungu atupee nabii mwingine,” alikamilisha Bw Sifuna.
Aliyekuwa mwakilishi wa Wadi ya Gatina, Bw David Ayoi alisema kuwa awali kulikuwa na walaghai ambao walitaka kumnyanganya nabii huyo shamba la Kawangware 56 ambalo alijenga kanisa la Jerusaleum of Christ Church.
Kiongozi huyo akisistiza mwili wa nabii huyo kuzikwa katika eneo hilo litapunguzia tamaa kwa wale wanaotaka kuliiba.
Bw Ayoi alinishika mkono bw Ayoi wanataka kuninyanganya shamba langu, wameninyanganya zingine huko nyumbani. Walizikizana kila kitu na hivyo akalipia kila kitu na kushughulikia.
“Hili shamaba ambalo wanateea mate, tutazika mama hapa ili ijulikane shamba ni la mama. Tutashika watoto wake mkono na kanisa liendelee,” alikamilisha Bw Ayoi.
Mary Sinaida Akatsa almaarufu kama Dada Mary au Mami, alizaliwa mwaka wa 1964 huko Bunyore.
Kulingana na familia yake, Akatsa alianza shule mwaka wa 1967 lakini aliacha masomo akiwa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi ya Etabalia.
Aliolewa na marehemu Francis Akatsa na ameacha wana wawili, David Jogoo na Moses Sangolo.