Mkenya Edwin Omindo anyakua Tuzo ya Safal ya Fasihi ya Kiswahili
Mwalimu na Mwandishi Edwin Omindo. Picha/Hisani
Kwa miaka mingi, mashindano ya fasihi hujulikana kwa majina makubwa kutoka Tanzania, lakini mwaka huu wa 2025, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jina moja kutoka Kenya liliibua shangwe na nderemo.
Hakuwa mwingine bali Edwin Omindo, mwalimu wa shule ya msingi kutoka Luanda katika Kaunti ya Vihiga.
Bw Omindo mnamo Alhamisi alitunukiwa dola 5,000 (sawa na Sh650,000) kwa muswada wake wa hadithi fupi wenye kichwa kisicho cha kawaida na ambacho ni ‘Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine’.
Usogora wake huo ndio uliomtambulisha si tu kama mshindi, bali kama mwandishi mwenye ucheshi, undani na ujasiri wa kuvuta msomaji kuanzia kichwa cha hadithi.
Katika orodha ya fainali ya Tuzo ya Safal ya Fasihi ya Kiswahili kwa mwaka 2024, Bw Omindo alikuwa ndiye Mkenya pekee, miongoni mwa majina saba yaliyoteuliwa kutoka mamia ya miswada iliyoletwa kutoka Afrika Mashariki.
Muswada wake ulishindana na kazi nyingine kutoka Tanzania. Kazi hizo ni pamoja na muswada wa ‘Kitanzi cha Mauti’ wake Mayasa Abdalla Chembea, ‘Bure Ghali’ wa Bashiru Abdallah, ‘Nderemo za Mtaa’, ‘Waadhi’, ‘Laana ya Uovu’ na 'Nyaraka za Wafu". Hata hivyo, Bw Omindo aling’aa katika kipengele cha hadithi fupi--na akaipa Kenya heshima ya kipekee.
Kwa upande wa Tanzania, Mayasa Abdalla na Bashiru Abdallah waliibuka washindi katika vipengele vya riwaya na ushairi mtawalia, kila mmoja akituzwa dola 5,000 (Tshs milioni 13).
Katika hotuba ya pongezi, Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Tanzania, Ashish Mistry, alisifu mchango wa Bw Omindo kwa kusema: “Kushinda kwake ni ishara kuwa vipaji haviko tu mijini au kwenye majukwaa ya kitaaluma--vipo hata mashinani, ndani ya madarasa ya shule za msingi.”
Mashindano haya yaliyoanzishwa mwaka 2014 na Dkt Lizzy Attree pamoja na Prof Mukoma wa Ngugi, hutoa jukwaa kwa waandishi wanaotumia lugha ya Kiswahili --lugha inayozidi kuenea, kubeba utambulisho, na kuunganisha watu wa tabaka zote.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo, Mwalimu Abdilatif Abdalla, alisisitiza kuwa kiwango cha ubora wa kazi zinazowasilishwa huimarika kila mwaka.
“Kuna mwamko wa kipekee wa ubunifu na umahiri miongoni mwa waandishi wanaojitokeza. Kiswahili sasa ni chombo cha fasihi za kisasa zenye uzito.”
Majaji, wakiongozwa na Dkt Salma Hamad, walikiri kuwa mwaka huu walipokea miswada iliyosheheni ubunifu, uhalisia wa maisha ya Kiafrika, na matumizi fasaha ya lugha.
Miswada inayoshinda huchapishwa na Mkuki na Nyota Publishers nchini Tanzania, hatua inayowahakikishia waandishi hao nafasi ya kuingia sokoni na kufikia wasomaji halisi.
Katika hafla hiyo ya Alhamisi, waliokuwepo walijumuisha viongozi wa serikali ya Tanzania, wakuu wa mikoa, wanataaluma, wanafunzi, wachapishaji, pamoja na wadau wa lugha na fasihi kutoka mataifa jirani.
Na kwa Edwin Omindo, mwalimu mnyenyekevu kutoka kijijini, huu ulikuwa ushindi wa roho, si tu kalamu.
Amedhihirisha kuwa si lazima uandike kutoka studio yenye kiyoyozi au maktaba ya kifahari ili kusikika barani Afrika.
Naam, Mungu hadanganywi. Na fasihi njema nayo haiwezi kufichwa.