Ufunguzi wa kituo cha upasuaji Utange afueni kwa wakazi
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir (kati) akijionea ndani ya Hospitali ya Kisasa ya Upasuaji iliyoko Utange, Mombasa. Picha/Mishi Gongo
Sekta ya afya katika Kaunti ya Mombasa imepigwa jeki baada ya kaunti hiyo kufungua kituo cha upasuaji katika eneo la Utange eneobunge la Kisauni.
Ufunguzi huo utasaidia pakubwa kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaohitaji upasuaji katika Hospitali Kuu ya Rufaa Makadara.
Aidha itapunguza hatua ambayo wakazi walilazimika kusafiri ili kupata huduma za upasuaji.
Ufunguzi wa kituo hicho uliongozwa na gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir, afisa mkuu wa hospitali ya Makadara Dkt Iqbal Khandwalla na viongozi wengine katika serikali ya kaunti ya Mombasa.
Khandwalla alisema kituo hicho kitasaidia pakubwa katika kupunguza msongamano na kutoa matibabu kwa muda ufaao.
Bi Mary Wambo, mmojawapo wa wazazi na ambaye mtoto wake alufanyiwa upasuaji baada ya ufunguzi wa kituo hicho, alieleza kuwa kituo hicho kimetoa afueni si kwa wazazi wenye watoto waliopasuka midomo tu bali hata wakazi watakaohitaji upasuaji aina nyingine.
"Kumekuwa na shida ya watu kupanga foleni katika hospitali kuu ya maji wa Mombasa kutafuta huduma za upasuaji.Wengi wamekuwa wakiumia kwa kukosa kutibiwa kwa muda unaofaa,kituo hicho kitasaidia kupunguza msongamano,"akasema.
Gavana Nassir alisema Hospitali hiyo ya kiwango cha Level 4 itakuwa ya kwanza kushughulikia upasuaji wa tatizo la kupasuka midomo kwa watoto wachanga.
“Kuanzia kaunti ya Kilifi hadi Mombasa hakuna hospitali ya umma inayoweza kufanya upasuaji huu hii itakuwa ya kwanza,Tumeianzisha ili kuwasaidia watoto waliopaasuka midomo," alisema.
Gavana pia alisema kaunti ya Mombasa ina mpango wa kutoa matibabu bila malipo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano licha ya mabadiliko ya bima mpya ya afya kutoka NHIF hadi SHA akiagiza maafisa husika kulifanikisha hilo katika hospitali zote za umma.
“Tulikuwa na mpango kila mtoto wa chini ya miaka mitano atibiwe bure katika hospitali za kaunti. Nadhani baada ya kuingia hii mambo ya SHA na SHIF kukawa na mchanganyiko wafanyakazi wa kaunti hakuweza kuelewa, sasa yale nimesema iweze kueleweka waziwazi hakuna mtoto yeyote wa chini ya miaka 5 ambaye ni wa Mombasa anastahili mzazi wake kulipishwa hata peni katika taasisi zetu za afya za kaunti.” Akasema.
Nassir pia alisema serikali yake ikishirikiana na wawakilishi Wadi na maafisa wa afya wa nyanjani na viongozi wengine watafanya zoezi la usajili wa bima mpya ya afya ya SHA kwa wakazi wa Mombasa akisema serikali hiyo aidha itawalipia wasiojiweza.