Visa vya watoto kunajisiwa na jamaa wa karibu vyaongezeka Kwale
Afisa wa masilahi ya watoto Msambweni, Kaunti ya Kwale, Bw Johnston Kivuli. Picha/Mishi Gongo
Idara ya watoto kaunti ya Kwale imeeleza hali ya wasiwasi kufuatia kuongezeka kwa visa vya watoto kudhulumiwa kimapenzi na jamaa zao wa karibu.
Akizungumza na AVDelta News kwa njia ya simu, afisa wa watoto eneo la Msambweni Johnston Kivuli alieleza kuwa wamerekodi zaidi ya visa 65 vya watoto kudhulumiwa kingono.
Kati yavyo, kuko na takriban 10 vinavyohusisha dhuluma na jamaa wa karibu kama baba, babu, na mjomba.
"Inasikitisha kuona watu wanaopaswa kuwalinda ndio wanaowadhulumu," akasema Bw Kivuli.
Afisa huyo alisema kwa sasa anashughulikia kesi mbili(2) za watoto waliodhulumiwa na baba wa kuwazaa kabisa.
Aidha alieleza kuwa vingi vya visa hivyo ni vile ambavyo wazazi wa kike wamesafiri kwenda kutafuta ajira ughaibuni na kuwaacha watoto na baba zao.
“Kwa sasa hivi nashughulikia kesi mbili(2) mahakamani za watoto ambao inadaiwa walidhulumiwa kingono na baba zao. Hizi ni kesi ambazo awali hazikuwa zinasikika lakini kwa sasa hivi tumeona hizi kesi zikiripotiwa kwa wingi katika afisi zetu,” alisema Bw Kivuli.
Kulingana na sheria ya kukomesha vitendo vya ukatili wa kingono, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumnajisi mtoto chini ya umri wa miaka tisa(9) anahukumiwa kifungo cha maisha jela, atakayepatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa umri wa miaka 13 hadi 15 anahukumiwa miaka 20 gerezani na atakayepatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa umri wa miaka 15 hadi 18 atahukumiwa miaka 15 gerezani.
Afisa huyo wa maswala ya watoto alisisitiza haja ya kuwepo na mikakati ya sheria ya kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama baada ya wazazi wao wa kike kusafiri Ughaibuni.
Wakati huo huo Bw Kivuli alikiri kuwepo kwa aina tofauti za visa vya dhuluma za kingono dhidi ya watoto.
“Kuna mkondo wa kwanza wa watoto dhidi ya watoto kudhulumiana kingono na aina ya pili ni watoto dhidi ya watu wazima. Hizi kesi zote tunazipokea na tunazishughulikia mahakamani. Kesi hizi ziko na mkondo tofauti hata ingawaje zinaanza mara tunapofahamishwa,” akasema.
Afisa huyo alisema kuwa idara ya watoto kwa ushirikiano na maafisa wa maswala ya watoto wa kujitolea nyanjani wanaendeleza kampeni za kuhamasisha jamii kuhusu kukomesha ukatili dhidi ya watoto.
Kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2021 na shirika la kimataifa la International Justice Mission (IJM) kwa ushirikiano na lile la Global Fund to End Modern Slavery, ulionyesha kuwa watoto takriban 7,000 katika kaunti za Kwale, Kilifi na Mombasa walihusishwa na ngono biashara.
Kenya ina kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kijinsia ambapo asilimia 15.6 ya wasichana na asilimia 6.4 ya wavulana wamepitia ukatili wa kijinsia wakati wa utoto wao, huku asilimia 13 ya wanawake wakiwa wamepitia ukatili wa kijinsia.
Bw Kivuli alisisitiza kuwa mkono wa sheria hautamuacha yeyote atakayepatikana na hatia ya kuwadhulumu watoto kingono.
Pia aliihimiza jamii kuripoti kesi hizo kwa wakati ili waathiriwa waweze kupata haki huku akisisitiza umuhimu wa haki sawa za kijinsia katika jamii.