Wanafunzi wa Kayole One wanufaika na mpango wa usalama barabarani
Picha ya pamoja ya Mkurugenzi wa Mipango katika Wakfu wa FIA Bi Agnieszka Krasnolucka akiwa na maafisa wa trafiki na wenzao wa Barabara za Mijini (KURA), walipotoa mafunzo kuhusu usalama barabarani. Picha/AVDelta News
Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kayole One, eneo la Embakasi ya Kati wamenufaika na mradi wa Safari Salama na Afya hadi Shuleni, unaolenga kupunguza ajali barabarani baada ya Wakfu wa FIA kwa ushirikiano na Halmashauri ya Barabara za Mijini Nchini (KURA) na mashirika mengine kuunda barabara zenye alama.
Hii ni kufuatia visa vya kuhuzunisha ambapo wanafunzi wanne walipoteza maisha yao kwenye barabara ya Kayole One karibu na makutano na barabara ya Spine.
Barabara hiyo iliwekwa njia ya miguu, na vivuko vya pundamilia ili kupunguza ajali. Itasaidia wanafunzi 3,800.
Mhadisi wa KURA Isaac Gitoho alisema ujenzi huo wa barabara hiyo iliyowekwa alama mbalimbali ulilenga kupunguza vifo ambavyo husababishwa na wenye pikipiki na magari.
“Vifo hivi hutokea kwa sababu hakuna nafasi ya kutumia kwa waendao kwa miguu. Ukiangalia hii shule, wanafunzi ni wengi na wanatumia hii barabara,” alisema Bw Gitoho.
Mkurugenzi wa Mipango katika Wakfu wa FIA Agnieszka Krasnolucka, alisema watoto huathiriwa punde tu ongezeko la magari linaposhuhudiwa. Bi Krasnolucka alisema barabara hiyo ya umbali wa mita 400 za njia ya kutembea, iligharimu Sh3.2 milioni kufanywa ya kisasa.
“Huu ni mradi unaolenga shule nyingi Barani Afrika. Lengo letu ni kuhakikisha maafa haya hayatokei tena siku zijazo. Katika wiki chache zilizopita, tumekuwa tukihamasisha wanafunzi umuhimu wa hatua za usalama zilizowekwa karibu na shule,” alisema Bi Krasnolucka.
Mkurugenzi wa Shirika la Amend nchini Tanzania na Afrika Bw Simon Kalolo alisema waathiriwa wengi wa ajali wanaotumia miguu ni wa umri kati ya miaka mitano(5) hadi 29. Alisema mradi huo utatekelezwa katika miji zaidi ya 10 katika nchi 10 Barani Afrika.
“Hapa tumejenga zaidi ya mita 400 za njia za watembeao kwa miguu zenye upana wa zaidi ya mita mbili(2), kutoa nafasi salama kwa watoto, watumiaji wa viti vya magurudumu, na wanaotembea kwa miguu wengine,” Bw Kalolo alisema.
Katika ripoti ya Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani (NTSA) 2024, inaonyesha kuwa watoto 424 wenye umri wa miaka kati ya mitano(5) hadi 19 walihusika kwenye ajali za barabarani.