Arsenal, Chelsea zaangukia wanyonge huku City ikipewa Liverpool robo fainali FA
- Created by Mwandishi AVDelta News
- Habari
Droo ya FA Cup yaleta pambano kubwa Etihad, timu ndogo zapata nafasi ya kushangaza vigogo.
Droo ya robo fainali ya FA Cup imewapa Arsenal na Chelsea mechi zinazoonekana kuwa rahisi, huku Manchester City wakipangwa dhidi ya Liverpool katika pambano kubwa la hatua hiyo.
Kwa mujibu wa droo iliyotangazwa Jumatatu, Arsenal watasafiri kucheza dhidi ya Southampton, wakati Chelsea watapambana na timu ya daraja la chini Port Vale.
Lakini macho ya mashabiki wengi sasa yanaelekezwa kwenye pambano la City dhidi ya Liverpool, ambalo tayari linatajwa kama “fainali kabla ya wakati.”
Timu hizo mbili zimekuwa miongoni mwa vigogo wakuu wa soka Uingereza katika muongo uliopita, na ushindi katika mechi hiyo unaweza kuwa hatua muhimu kuelekea nusu fainali.
Robo fainali nyingine itawakutanisha Leeds United na mshindi kati ya West Ham United au Brentford.
Droo kamili ya robo fainali FA Cup:
- Manchester City vs Liverpool
- Southampton vs Arsenal
- Port Vale vs Chelsea
- West Ham United / Brentford vs Leeds United
Kwa Port Vale na Southampton, droo hii inaleta matumaini ya kufanya maajabu dhidi ya vigogo wa Ligi Kuu ya Uingereza.
Washindi wa mechi hizi watasonga mbele hadi nusu fainali zitakazochezwa katika Wembley Stadium, hatua moja tu kabla ya fainali ya kombe hilo maarufu la Uingereza.
Droo hiyo inazipa Arsenal na Manchester City matumaini ya kutimiza ndoto ya kushinda zaidi ya taji moja.
Timu hizo mbili zitakutana fainali ya kombe la Carabao Machi 22, huku kuanzia Jumanne zikishiriki mkondo wa kwanza wa raundi ya 16 UEFA Champions League.
Aidha, zinafuatana kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal ikiwa mbele kwa alama saba, lakini Cuty wako na mechi moja mkononi.