Bunge laagiza mwanafunzi aliyefukuzwa kwa kuvaa hijabu arudishwe shuleni
- Habari
Prof Bitok akiri mwanafunzi hayuko shuleni, PAC yasisitiza arudi mara moja.
Kamati ya Bunge kuhusu Fedha za Umma (PAC) imeagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha mwanafunzi Muislamu wa Gredi ya Kumi katika shule ya St Mary’s Lwak Girls, Kaunti ya Siaya, anarudishwa darasani mara moja.
Agizo hilo lilijiri Alhamisi baada ya kuripotiwa kuwa msichana huyo alifukuzwa kwa kuvaa hijabu katika shule inayosimamiwa na kanisa.
Suala hilo liliibuka katika kikao cha kamati hiyo baada ya Mbunge wa Kike Kaunti ya Garissa na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Bi Amina Udgoon Siyad, kueleza kuwa mwanafunzi huyo, Samira Ramadhan, alinyimwa ruhusa ya kuvaa hijabu licha ya kuahidiwa wakati wa kuandikishwa kuwa angeruhusiwa.
“Licha ya kuhakikishiwa wakati wa usajili kwamba angevaa hijabu, sasa hawezi kuendelea na masomo. Juhudi za baba yake kutafuta maelezo kutoka kwa uongozi wa shule hazijafanikiwa,” alisema Bi Siyad.
Katiba iko wazi
Mbunge wa Teso Kusini, Mary Emaase, alinukuu Ibara ya 27 ya Katiba ya Kenya inayohusu usawa na kutobaguliwa.
“Kila mtu ni sawa mbele ya sheria na ana haki ya ulinzi sawa. Serikali haitabagua kwa misingi ya dini,” alisema Bi Emaase.
Mbunge wa Rarieda, Dkt Otiende Amollo, alisisitiza umuhimu wa kupata ukweli kamili wa tukio hilo, lakini akasema mwanafunzi hawezi kuendelea kukaa nyumbani.
“Suala hili ni nzito. Sheria iko wazi. Lakini tunahitaji taarifa kamili. Hata hivyo, mtoto hawezi kubaki nyumbani tukisubiri uchunguzi,” alisema.
Wizara yaahidi hatua ya haraka
Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Butere, Tindi Mwale, alimhoji Katibu Mkuu wa Elimu ya Msingi, Prof Julius Bitok, kuhusu hali ya mwanafunzi huyo.
Prof Bitok alikiri kuwa mwanafunzi huyo hakuwa shuleni lakini akaahidi hatua za haraka.
“Msichana aliondolewa shuleni. Nitahakikisha anarudi mara moja, hata leo,” akasema.
Aliongeza kuwa taarifa kutoka ofisi ya elimu ya eneo na shule zinakinzana, hivyo kuhitaji uchunguzi zaidi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakuna ubaguzi unaoruhusiwa kwa misingi ya dini.
“Sheria iko wazi. Haipaswi kuwa na ubaguzi wa aina yoyote kwa misingi ya dini,” akasema Prof Bitok.