Skip to main content Skip to page footer

Hatimaye Mombasa wamefikiwa: Garimoshi jipya kuzinduliwa kwa abiria wa treni za SGR

Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, alipokagua mradi huu wiki iliyopita, alisema reli iko tayari na inatarajiwa kuhudumia abiria wapatao 4,000 kwa siku.

Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir (wa nne kushoto) aonja usafiri wa garimoshi kati ya kisiwa cha Mombasa na kituo cha SGR kilichoko Miritini. Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua rasmi ucukuzi huo Septemba 17, 2025. Picha/Kenya Railways

avdeltanews@gmail.com

Hatimaye wanaotumia garimoshi la Madaraka Express watapata usafiri wa kuunganisha kati ya kituo cha Miritini na katikati ya jiji la Mombasa.

Huduma hii ya Mombasa Commuter Rail inaanza rasmi leo Jumatano, Septemba 17, 2025.

Mradi huu ambao umegharimu takribani Sh4.2 bilioni umehusisha ukarabati wa takribani kilomita 16.6 za reli ya zamani ya ‘metre gauge’ na ujenzi wa miundombinu muhimu.

Hiyo ni pamoja na daraja la urefu wa kilomita 2.3 juu ya Makupa Causeway.

Vituo vipya na vilivyokarabatiwa katika maeneo ya Miritini, Changamwe West, Changamwe East, Shimanzi, Mazeras na katikati ya jiji vimekamilika, sambamba na huduma za “Kuegesha na Kuondoka” na “Kushukisha and Kuondoka”.

Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, alipokagua mradi huu wiki iliyopita, alisema reli iko tayari na inatarajiwa kuhudumia abiria wapatao 4,000 kwa siku.

Kulingana naye, hatua hiyo itapunguza msongamano mkubwa wa magari barabarani kati ya Miritini na Changamwe.

Huduma hii inatoa mbadala wa uhakika kwa abiria wanaowasili kwa Madaraka Express, ambao kwa sasa wanalazimika kutumia matatu, teksi au bodaboda kuingia mjini.

Hali kama hii imekuwa ikifanikishwa kwa muda mrefu jijini Nairobi, ambapo huduma ya commuter rail kati ya kituo cha Syokimau na katikati ya jiji imewasaidia maelfu ya abiria kufika mjini kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Nauli ya kati ya kituo cha Miritini na katikati ya jiji la Mombasa imepangwa kuwa Shilingi 50 pekee. Ni kiwango sawa na cha Nairobi, kitakachohakikisha huduma hii inabaki nafuu kwa wakazi.

Shirika la Reli Nchini linasema mradi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari, gharama za usafiri kwa abiria wa kila siku, na pia kupunguza msongamano wa magari barabarani.

Ujenzi umekamilika na majaribio ya usalama yamefanyika.

Changamoto za awali, hasa za fidia za ardhi, zilitatuliwa baada ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi kupokea Shilingi 1.1 bilioni kwa ajili ya ulipaji.

Kinachosubiriwa sasa ni uzinduzi rasmi utakaofanywa na Rais William Ruto.

Kwa wakazi wengi wa Mombasa, hii ni hatua ya kihistoria katika kubadilisha namna ya kusafiri mjini, kuboresha muunganiko wa mijini na kutoa uzoefu rahisi na wa kuaminika kwa maelfu ya watu wanaosafiri kila siku kutoka pembezoni hadi katikati ya jiji.