Skip to main content Skip to page footer

IEBC yaonya huenda baadhi ya chaguzi ndogo zisifanyike kwa uhaba wa pesa

Tume yasema kati ya bajeti ya Sh1.046 bilioni iliyotengwa kufanikisha chaguzi ndogo 24, ni Sh788 milioni pekee zilizotolewa na Hazina ya Taifa.

Marjan Hussein Marjan

Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Marjan Hussein Marjan alipofika mbele ya kamati ya Bunge mnamo Septemba 18, 2025. Picha/PBU

avdeltanews@gmail.com

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeonya kuwa huenda ikashindwa kuendesha chaguzi ndogo zote zilizopangwa kufanyika Novemba 27, 2025, kutokana na uhaba wa fedha.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Hesabu za Umma (PAC) ya Bunge mnamo Jumatano, Afisa Mtendaji Mkuu wa IEBC, Bw Marjan Hussein Marjan, alisema kuwa kati ya bajeti ya Sh1.046 bilioni iliyotengwa kufanikisha chaguzi ndogo 24, ni Sh788 milioni pekee zilizotolewa na Hazina ya Taifa.

Hii imeruhusu kufanyika kwa chaguzi ndogo 16 pekee, huku nyingine nane zikisalia bila ufadhili.

“Tunaendesha chaguzi zote ndogo, lakini zingine zilitambuliwa baadaye baada ya fedha kwa zile 16 za mwanzo kupitishwa,” alisema Bw Marjan.

“Tunaendelea kuzungumza na Hazina ya Taifa kufungua fedha zaidi kwa dharura kwa hizo nane.”

Tume iliongeza kuwa ucheleweshaji wa manunuzi pia unazua wasiwasi, kwa kuwa lazima ifuate mfumo wa kielektroniki wa serikali wa manunuzi (e-GP).

Hadi sasa, vifaa muhimu vya uchaguzi kama karatasi za kura na sajili bado havijanunuliwa, ingawa mafunzo ya watumishi tayari yamekamilika.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Edung Ethekon, alisisitiza kuwa chaguzi zote 24 zitaendelea kufanyika Novemba 27, ikiwemo Banissa, ambayo haina mbunge tangu 2022.

“Ndiyo maana tulipanga tarehe 27 Novemba, tukiamini inatoa muda wa kutosha iwapo fedha zitatolewa kwa wakati,” alisema Bw Ethekon.

“Wakenya watashuhudia chaguzi ndogo za kuaminika zitakazokuwa majaribio muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.”

Wakati huohuo, IEBC ilitangaza kuanza kwa usajili wa wapiga kura kuanzia Septemba 29, 2025.

Tume inalenga kusajili wapigakura wapya zaidi ya milioni 6.3, ambapo asilimia 70 wanatarajiwa kuwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 34.

Usajili huo utafanyika katika ofisi za kila eneobunge na katika vituo 57 vya Huduma Centre kote nchini, pamoja na kwa Wakenya walioko ughaibuni almaarufu Diaspora.

Bw Ethekon alieleza kuwa sajili hiyo mpya itakaguliwa na kusafishwa ili kuondoa majina ya waliofariki na yaliyodurufu.

“Uadilifu wa sajili ya wapiga kura ni kiini cha chaguzi za kuaminika, na tumejizatiti kuhakikisha ni sahihi na salama,” alisema.

Hata hivyo, suala la mapitio ya mipaka ya maeneo ya uchaguzi bado halijashughulikiwa kikamilifu, licha ya IEBC kupokea mwongozo kutoka Mahakama ya Juu.

Baadhi ya wabunge, akiwemo Mohamed Adow wa Wajir Kusini, waliitaka Tume kuharakisha mchakato huo ili kuhakikisha usawa katika uwakilishi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Funyula, Dkt Wilberforce Oundo, alionya kuwa joto la kisiasa linaongezeka kuelekea uchaguzi wa 2027 na akasisitiza kuwa chaguzi ndogo zikishindwa kusimamiwa ipasavyo, zinaweza kusababisha vurugu.

“Vurugu za uchaguzi zinaweza kutumbukiza taifa hili katika machafuko,” alisema Dkt Oundo.

“Chaguzi hizi lazima zioneshe kuwa vurugu za kisiasa zinaweza kudhibitiwa.”

Bw Ethekon, hata hivyo, alisisitiza kuwa jukumu la kudumisha amani si la IEBC pekee bali ni la pamoja kwa wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi.

Tangu kuchukua usukani mapema mwaka huu wa 2025, Bw Ethekon ameahidi kutoruhusu udanganyifu katika uchaguzi wa 2027, akiahidi uwazi na kuimarisha udhibiti wa ndani wa Tume hiyo.