AVDelta News
Skip to main content Skip to page footer

Kalonzo awasili Washington kwa maombi huku siasa za Azimio zikichukua mkondo wa kimataifa

Kwa wanaofuatilia siasa, kualikwa kwa Kalonzo ni ishara ya kutambuliwa kwake kimataifa. 

thenamlola@gmail.com

Kiongozi wa Wiper Party, Kalonzo Musyoka, amewasili nchini Marekani kwa sherehe ya 74 ya Maombi ya Kitaifa.

Kalonzo ambayo wiki hii alipewa mikoba ya kuongoza muungano wa Azimio, alisambaza picha kwenye mtandao wake wa Facebook akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles, jijini Washington DC.

Akizungumza baada ya kuwasili, Kalonzo aliwashukuru Albina, Shanice na Enrique kwa ukarimu waliouonyesha.

"Natarajia kuwa na  mazungumzo yenye tija na Wakenya wanaoishi Marekani pamoja na viongozi wengine duniani," akaandika.

Kiongozi huyo aliandamana na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye ni mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, pamoja na Seneta wa Kaunti ya Makueni, Dan Maanzo.

Maombi hayo ya Kitaifa ya Asubuhi nchini Marekani hufanywa kila mwaka. Huwaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kidiplomasia na wa kidini kujadili masuala ya uongozi, maadili na ushirikiano wa kimataifa.

Kwa wanaofuatilia siasa, kualikwa kwa Kalonzo ni ishara ya kutambuliwa kwake kimataifa. Inampa fursa ya kueleza sera zake kwa wakuu wa Marekani na Wakenya waishio huku, ikisalia miezi 16 kabla ya Uchaguzi mkuu wa 2027.

Ingawa Muungano wa Upinzani haujaonyesha ishara ya kiongozi unayeoanga kumkabidhi funguo za kufungua milango ya ikulu, kukwezwa kwa Kalonzo kusimamia Azimio kunampa kauli nyumbani na kimataifa.

Kuandamwa kwake na siasa za serikali katika siku chache zilizopita, kunaashiria mti wenye matunda kurushiwa mawe.

Mitandaoni,  kumekuwa na tetesi kuwa Kalonzo amealikwa kukutana na Rais Donald Trump, lakini huo ni uvumi ambao ikulu ya White House haijaukana wala kuthibitisha.

Kilicho wazi ni kwamba, si kila mtu hualikwa kwenye hafla za kimataifa. Safari hii ni zamu ya  kiongozi huyo wa Wiper, ambaye kwa mara ya kwanza tangu 2007, ameonyesha nia ya kutaka kuwa rais wa Kenya.

Amewahi mara mbili (2013 na 2017) kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga kupitia miungano na Cord na NASA.

Ingawa mnamo 2022 Raila aliamua kwenda na Martha Karua kama mgombea mwenza wa Azimio,  Kalonzo hakutangaza kuhama muungano hio au kuwania urais kivyake.

Kwa wafuasi wake, yeye ndiye mwanasiasa mwenye tajriba zaidi miongoni mwa viongozi wa Muungano wa Upinzani.

Kwa sasa, 2027 bado ipo mbali, na Kalonzo anaendelea kujitambulisha na kuimarisha nafasi yake kwa wapiga kura nchini na nje ya Kenya.

Kalonzo in the US
Kiongozi wa Wiper na Azimio Kalonzo Musyoka alipowasili jijini Washington, D.C., Marekani. Picha/Hisani