Skip to main content Skip to page footer

Kesi ya Shakahola: Shahidi asimulia kumuokoa mvulana aliyetoroka mateso

Zaidi ya washukiwa 35 walibainishwa kupitia uchunguzi huo.

Mahakama

Mahakama ya Watoto ya Tononoka, Mombasa. Shahidi asema aliokoa mtoto aliyetoroka mateso Picha/Maktaba

avdeltanews@gmail.com 

Kesi dhidi ya mhubiri tata Paul Nthenge Mackenzie na washitakiwa wenzake 35 iliendelea Jumatano katika Mahakama ya Watoto ya Tononoka mbele ya Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir, ambapo mashahidi waliendelea kusimulia simulizi za kusikitisha kuhusu mauaji ya Shakahola.

Mashahidi walieleza visa vya watoto kupotea, familia kuteketea, na ushahidi wa kisayansi kuthibitisha utambulisho wa miili iliyofukuliwa.

Khadija Wilson, 26, alisimulia jinsi yeye na kaka yake mdogo walivyomuokoa mvulana mdogo aliyejulikana kama P.P. wakiwa eneo la Madukani Shakahola.

 Khadija alisema mtoto huyo alikuwa ametoroka kwenye mafundisho ya Mackenzie ambako alilazimishwa kufunga na kudhoofika sana.

Alimlea karibu miezi minne baada ya kumuarifu mzee wa kijiji, ambaye aliwajulisha maafisa wa watoto. 

Hatimaye, mtoto huyo alipelekwa chini ya uangalizi wa serikali.

 “Kama hatungemwokoa, angefariki,” alisema mahakamani, akiongeza kuwa wakati wa kumwokoa, P.P. hakuwa na nguvu hata za kuhudhuria shule.

Mzee Charles Adundo alieleza kuwa mjukuu wake alichukuliwa kutoka shuleni na mtoto wake wa kiume — ambaye sasa ni mshtakiwa wa 35 — na hajawahi kuwaona tena.

Mashahidi wengine akiwemo Bi Felida Vugusa, 70, kutoka Kapseret, waliambia mahakama jinsi binti yake, Sarah Khahisha, na watoto wake watano walivyotoweka ghafla pamoja na mume wake Mulama.

Bi Felida alisema familia hiyo ilikuwa imeanza kuhudhuria kanisa lisilojulikana, na Mulama alikuwa akipinga kabisa watoto kwenda shule.

Ushahidi wa kitaalamu uliwasilishwa na Bw Henry Kiptoo, mchambuzi wa serikali katika Maabara ya Serikali Nairobi.

 Alieleza kuwa walichunguza sampuli 333 kutoka kwa familia zilizopoteza ndugu na kutayarisha ripoti mbili — tarehe 6 Agosti 2024 na 13 Novemba 2024 — zilizothibitisha miili 38 na 31 mtawalia, baadhi ikiwa ya watoto na jamaa wa washitakiwa.

Bw Liwa Filbert, Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Taifa, naye alieleza jinsi walivyotumia alama za vidole kuthibitisha utambulisho wa washukiwa waliotoa majina ya uongo. 

Zaidi ya washukiwa 35 walibainishwa kupitia uchunguzi huo.

Kesi iliahirishwa hadi 19 Septemba 2025 kuendelea.