AVDelta News
Skip to main content Skip to page footer

Kewasnet yataka serikali kuboresha huduma za maji nchini

  • Ufisadi katika sekta ya maji watajwa kuwa chanzo cha Wakenya kukosa maji safi.

Muungano wa mashirika ya kutetea haki ya upatikanaji wa maji na usafi nchini (Kewasnet) umeelezea wasiwasi wao ukisema serikali imeshindwa kutoa huduma za maji safi na kuimarisha usafi wa mazingira katika maeneo mengi nchini Kenya.

Wawakilishi wa muungani huo ambao walikuwa na kikao cha siku mbili(2) katika eneo la Diani kaunti ya Kwale, kujadiliana kuhusu uwajibikaji wa serikali za kaunti kuhusiana na huduma za maji, walisema inasikitisha kwamba rasilimali hiyo muhimu haitunzwi ipasavyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Kewasnet--Kenya Water and Sanitation Civil Society Network--Malesi Shivaji alisema kuwa ni sharti uwajibikaji wa maji na usafi wa mazingira nchini Kenya uimarishwe.

Mkurugenzi huyo alieleza kusikitishwa na hali duni ya mazingira na baadhi ya wakazi maeneo mbalimbali nchini kutopata maji safi ya kunywa.

“Kushindwa kwa uwajibikaji kunaiwacha jamii na ukosefu wa ufahamu na utaratibu wa kutatua malalamiko yao dhidi ya serikali kushindwa kutimiza haki zao za maji na usafi wa mazingira,” alisema Shivaji.

Kulingana na ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Umma (KIPPRA ), kaunti nyingi zinakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa kiufundi na rasilimali duni za usimamizi na uangalizi bora wa kifedha.

Aidha Shivaji alisema kwamba licha ya mifumo ya kisheria kuwepo, kuna migogoro mikubwa ambayo baadaye inazuia utekelezaji mzuri wa kutoa huduma kwa wananchi.

“Kushindwa kutoa maelezo ya wajibu ulioidhinishwa na katiba, kunasababisha ukosefu wa uelewa juu ya maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa au msaada ambao unaweza kutolewa nawashirika ,” akasema Shivaji.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la CESPAD Ashah Shaaban alieleza masikitiko yake ya wananchi kupata huduma duni za maji hivyo akiitaka serikali kuu na zile za kaunti kubuni utaratibu wa kutoa Data ya wakati halisi ya sekta ya maji ambayo umma unaweza kuipata na ambayo inaweza kutumika kufanya maamuzi kwa wakati ufaao.

"Data itaeleza maeneo ambayo yanahitaji hatua za dharura kuwapatia wakazi maji safi ya kunywa,"akaeleza.

Kadhalika alizitaka serikali za kaunti zitekeleze kikamilifu mamlaka yao ya kuhifadhi udongo na maji ,kaunti zifuate miongozo ya ushiriki wa umma ili kuongoza utendakazi wake pamoja na kuchukua jukumu kuu katika uratibu wa washirika na shughuli za sekta tofauti kubwa na sekta ndogo.

Shaban aidha alizitaka serikali za kaunti kutekeleza kikamilifu mwongozo wa utoaji wa huduma za maji vijijini kama ulivyoratibiwa na bodi ya uthibiti wa huduma za maji nchini WASREB.

Akigusia swala la ufisadi, mkurugenzi wa shirika la Kenya Water For Health Organisation (KWAHO) Patrick Alubbe alitaja kuwa ufisadi katika sekta ya maji kuwa chanzo cha Wakenya kukosa maji safi.

"Ufisadi katika sekta ya maji ndo unaozuia wakazi katika maeneo mengi nchini kupata maji safi ya kunywa.Kama unastahili unisambazie maji na umefeli huo tayari ni ufisadi,"akasema.

Aliongezea kuwa kuna mengi ambayo yanaendelea katika sekta ya maji ambayo yanahitaji kurekebishwa.

 "Pesa zile za maji zinazokuja kwa kaunti mara nyingi huwa ni pesa za kutosha ila zinapofika katika mabunge ya kaunti kila mwakilishi wadi anataka apewe pesa kidogo , kwa hio tunataka kaunti zieke kipao mbele miradi ya maji inayopania kutekeleza badala ya kueka miradi ya maji kila sehemu yenye gharama za juu ambayo wakaazi hushindwa na kuitunza hivyo kukosa kufaidika ,”akasema Alubbe.

Tangu kuanza kwa serikali za ugatuzi sekta ya maji ni kati ya wizara kuu zinazotengewa mgao mkubwa wa fedha kila mwaka wakifedha na serikali za ugatuzi.

Hata hivyo asilimia kubwa ya wakaazi wanaendelea kukumbwa na uhaba wa maji ,baadhi yao wakilazimika kununua bidhaa hiyo kwa bei za juu huku walala hoi wakisalia kutumia maji ya mto na visima ambayo sio salama.

Maafisa katika muungano wa kupigania upatikanaji wa maji safi nchini walipokongamana katika eneo la Diani, Kaunti ya Kwale. Picha/Mishi Gongo