Mashujaa Dei 2025: Raila Odinga asalia kwa nyoyo za viongozi na raia
Rais William Ruto na mgeni wake Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal katika uwanja wa Ithookwe, Kitui. Picha/PCS
Sherehe za kitaifa za Sikukuu ya Mashujaa mwaka huu, zilizofanyika Jumatatu, Oktoba 20, 2025, katika Uwanja wa Ithookwe, Kaunti ya Kitui, zilichukua sura ya kipekee na yenye hisia nzito.
Taifa zima liliungana kumkumbuka na kumuenzi marehemu Raila Amolo Odinga, kiongozi wa chama cha ODM na Waziri Mkuu wa zamani, aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini India.
Kwa mara ya kwanza tangu kifo chake, majina ya mashujaa waliochangia historia ya Kenya yaliposomwa, umati uliibua shangwe na machozi kwa pamoja lilipotajwa jina la Raila Odinga — mwana wa waziri wa kwanza wa nchi, Jaramogi Oginga Odinga, na nembo ya mapambano ya pili ya ukombozi wa taifa.
Rais William Samoei Ruto, akihutubia maelfu ya wananchi, viongozi wa kisiasa na wageni wa heshima kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, alimtaja Raila kama “shujaa wa kizazi chetu,” akisema mchango wake katika ujenzi wa taifa hauwezi kufutika.
“Tunapoadhimisha mashujaa wetu, tunamkumbuka pia marehemu Raila Amolo Odinga — mtu aliyejitolea kwa dhati kupigania demokrasia, haki na usawa,” alisema Rais Ruto. “Raila alisimama na taifa katika nyakati ambazo wengi wangesalimu amri. Alipigania katiba, usawa wa kijamii, na heshima kwa kila Mkenya, bila kujali dini, kabila, au hadhi.”
Rais Ruto aliongeza kuwa Raila alikuwa kiongozi mwenye maono ya maendeleo, aliyegusa sekta mbalimbali za uchumi na maisha ya wananchi.
Alimtaja kama mwanamageuzi wa kweli katika sekta ya kawi na miundombinu, akisema juhudi zake kama Waziri wa Nishati na baadaye Waziri wa Barabara, Nyumba na Umwagiliaji zilisaidia kuweka msingi wa miradi mikubwa ya kitaifa.
“Tukumbuke kuwa Raila ndiye alianzisha mageuzi makubwa katika sekta ya kawi — kuimarisha uzalishaji wa umeme wa maji na jotoardhi, na kufanikisha mradi wa Olkaria ulioleta mapinduzi ya nishati safi nchini. Pia alihamasisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ikiwemo barabara kuu za jiji na upanuzi wa Bandari ya Mombasa,” alisema Rais Ruto, huku akipigiwa makofi.
Katika hotuba yake, Rais Ruto alisisitiza kuwa ushujaa wa Raila haukuwa wa kisiasa pekee, bali pia wa kimaadili na kiutu.
Alimuelezea kama mtu aliyeamini katika maridhiano na upatanisho, hasa baada ya mivutano mikubwa ya uchaguzi, akisema alionesha mfano wa kiongozi anayechagua amani badala ya visasi.
“Wengi hawataisahau Handshake ya 2018, ambayo ilirejesha utulivu na umoja wa taifa. Raila alionyesha kwamba Kenya ni kubwa kuliko mtu mmoja. Huo ndio urithi wa kweli wa ushujaa,” aliongeza Rais.
Zaidi ya hayo, serikali ilimtunuku marehemu Odinga tuzo ya Chief of the Order of the Golden Heart of Kenya (CGH) — heshima ya juu zaidi inayotolewa kwa raia kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Katika uwanja wa Ithookwe, hewa ilikuwa nzito kwa hisia. Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walitumbuiza kwa nyimbo na maigizo yaliyomuenzi Raila, wakimwita “Tinga wa Kenya” — jina lililomtambulisha tangu akiwa kijana kutokana na upendo wake kwa mitambo na magari mazito ya ujenzi.
Wengi walieleza kwamba jina hilo, “Tinga,” lilitokana na ujasiri wake wa “kusukuma” mabadiliko licha ya upinzani, kama vile trekta lisilozimika.
Viongozi kadhaa wa Afrika pia walitoa salamu za rambirambi.
Waziri Mkuu wa Msumbiji Maria Benvinda Levi alisema Raila “alitetea Afrika yenye haki na utu.”
Bi Maria alitoa rambirambi za Rais Daniel Fransisco Chapo ambaye pia aliyngana na ulimwengu kutambua ushujaa wa Raila.
Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye ambaye alikuwa mgebi rasmi, alimtaja Raila kuwa kiongozi aliyeamini Afrika inaweza kusimama bila msaada wa kigeni.
Gavana wa Kitui, Dkt Julius Malombe, alitaja Raila kama “mwanasiasa jasiri, aliyeishi kwa ajili ya wengine.”
Kando na hotuba, wananchi wengi walihusishwa na matukio ya kumbukumbu yaliyofanyika kote nchini — ikiwemo upandaji miti elfu kumi kwa jina la Raila katika kaunti mbalimbali, kama ishara ya urithi wa matumaini na uhai wa taifa.
Rais Ruto alihitimisha kwa kusema, “Mashujaa kama Raila hawafi — wanaendelea kuishi kupitia maadili na kazi walizoacha. Tunaposherehekea Mashujaa Dei, tumejifunza kwamba ushujaa ni kusimama kwa haki, hata unapokuwa peke yako.”
Raila Odinga alizikwa Jumapili, nyumbani kwake Opoda Farm, Bondo, Kaunti ya Siaya, katika mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mazishi hayo yalitawaliwa na hisia, nyimbo za mapambano, na kumbukumbu za maisha ya mtu aliyepigania taifa hadi pumzi yake ya mwisho.