Mbunge wa zamani apinga mpango wa kulipisha barabara ya Dongo Kundu
Mwakilishi wa Kike wa zamani Kaunti ya Kwale, Bi Zuleha Juma Hassan katika picha ya awali. Amepinga barabara ya Dongo Kundu kuwa ya kulipia. Picha/Hisani
Mwakilishi wa Kike wa zamani Kaunti ya Kwale, Bi Zuleikha Juma Hassan, ametoa wito kwa Rais William Ruto kutopitisha pendekezo la kuifanya barabara ya Dongo Kundu kuwa barabara ya kulipia.
Amesema hatua hiyo itadhoofisha uchumi wa eneo hilo na kuwabebesha wakazi mzigo usiokuwa wa lazima.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Bi Zuleikha alisema barabara ya Dongo Kundu ni kiungo kinachorahisisha usafiri katika kipindi ambacho barabara ya Kinango–Kwale bado haijakamilika.
“Naomba Rais asipitishe rai hiyo ya kutoza kodi. Tunataka barabara hii ifunguliwe rasmi ili wananchi wote waweze kuitumia pamoja na vyombo vya usafiri wa umma bila hofu ya kulipia. Tuwe huru kama Wakenya wengine ambao wamejengewa barabara mpya katika kaunti zao na wanazitumia bila kutozwa,” alisema.
Bi Zuleikha alisisitiza kuwa iwapo serikali itaruhusu barabara hiyo itumike bure kwa sasa, mapato yatarejea kupitia ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
“Kodi wanayotaka kuipata haitatoka kwa kutoza magari; italipwa na biashara zitakazopanuka, ajira zitakazozuka, na uchumi utakapoimarika. Lakini kutoza kodi mapema kutazorotesha uchumi wa Kaunti ya Kwale na kuwaumiza wananchi,” aliongeza.
Mradi wa Dongo Kundu Bypass ni mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya miundombinu nchini, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
Umeundwa kupunguza msongamano katika kivuko cha Likoni na kufungua fursa za kiuchumi kwa kaunti za Mombasa, Kwale na Taita Taveta, kupitia uhusiano wa moja kwa moja kati ya Bandari ya Mombasa na barabara ya Mombasa–Lunga Lunga.
Awamu ya kwanza ya mradi, yenye urefu wa kilomita 11 kutoka Miritini hadi Mwache, tayari imekamilika, huku awamu zinazofuata zikikaribia kukamilishwa.
Serikali imependekeza kuifanya barabara hiyo kuwa ya kulipia, ili kusaidia matengenezo na kufidia gharama za ujenzi.
Hata hivyo, viongozi wa Pwani, akiwemo Bi Zulekha, wanasema wakazi hawapaswi kubebeshwa mzigo wa ada mpya kabla ya kunufaika na faida kamili za mradi huo.
“Serikali ikitaka kukuza uchumi wa Kwale, basi ianze kwa kuwapa wananchi uhuru wa kuitumia barabara hii. Hiyo ndiyo njia pekee ya uchumi kuzaa,” alisema.