Pwani wafurahia usafiri wa reli kutoka mjini
Rais William Ruto akifungua ubao wa kuashiria uzinduzi rami wa treni ya kuunganisha abiria kati ya Miritini na Mombasa mjini. Picha/Hisani
Hatimaye wanaosafiri kwa garimoshi la Madaraka Express wamepata afueni baada ya kuzinduliwa kwa treni mpya ya Mombasa Commuter Rail.
Treni hiyo inaunganisha Kituo cha Reli cha Mombasa mjini na Kituo cha SGR Miritini.
Mradi huo unatarajiwa kubeba abiria wasiopungua 4,000 kwa siku. Pia unatarajiwa kurahisisha safari na kupunguza gharama kubwa za usafiri ambazo kwa muda mrefu zimekuwa changamoto kwa wakazi wa Pwani.
Wanafunzi, wafanyakazi na wafanyabiashara sasa wanaona hiyo reli kama suluhisho la kudumu la foleni na nauli za juu barabarani.
Katika hafla ya uzinduzi, viongozi wa kitaifa na wa eneo hilo walikusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu.
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir alitumia mfano wa mwanamke aliye na uchungu wa uzazi anayemlaumu mume wake wakati wa maumivu lakini kisha kumsamehe baada ya kupata mtoto, akiwataka wakaazi wa Pwani kutambua manufaa ya mradi huo.
“Unaporahisisha watu na bidhaa zao kusafiri, wewe umejenga uchumi. Binadamu tuna tabia ya kusahau, lakini najikumbusha na kuwakumbusha tusilisahau hili,” alisema.
Waziri wa Uchimbaji Madini na Uchumi wa Bahari Hassan Joho naye alisema kwamba kwa mara ya kwanza chini ya Rais William Ruto, Pwani inajihisi kujumuishwa katika ajenda ya maendeleo ya taifa.
Bw Joho aliwahimiza wananchi kushirikiana na serikali, akiwasisitizia kuitikia kauli ya “two-term,” akisema serikali sasa imefanya kwa Pwani kile ambacho awali kilionekana kufanywa kwa wengine tu.
Rais William Ruto alisema hiyo treni mpya ni hatua kubwa ya kuwawezesha kiuchumi wakazi wa Mombasa kwa kuwapatia njia nafuu, salama na ya haraka ya usafiri kati ya jiji na vituo vya biashara.
“Tumehakikisha kuwa nauli ni ya chini kabisa ili kila Mkenya aweze kusafiri. Safari kutoka Mombasa mjini hadi Miritini itagharimu shilingi 50 pekee, na safari kamili kutoka Nairobi hadi Mombasa kwa kutumia SGR na commuter rail haitazidi shilingi 1,000,” alisema.
Aliongeza kuwa hiyo ni njia ya kupunguza mzigo wa maisha kwa wananchi.
Aidha, Rais aliahidi kuwa atarudi Mombasa kuendeleza eneo maalumu la kiuchumi la Dongo Kundu na upanuzi wa Bandari ya Mombasa.
"Dhamira ya serikali ni kuimarisha nafasi ya Pwani katika uchumi wa taifa," akasema.
Treni hiyo mpya, iliyozinduliwa zaidi ya miaka 130 baada ya reli ya kwanza ya Uganda kuletwa nchini, inaleta mageuzi makubwa ya usafirishaji mjini Mombasa.
Kwa muda mrefu, abiria waliokuwa wakisafiri kwa SGR kutoka Nairobi walipata changamoto kubwa kufika katikati ya jiji kutokana na gharama kubwa na foleni ya barabara kutoka Miritini.
Sasa reli ya mita (Metre Gauge Railway) iliyokuwepo imekarabatiwa na kuunganishwa na kituo cha SGR kupitia madaraja, njia mpya na vituo vipya vya abiria katika Shimanzi, Changamwe na Miritini.
Shirika la Reli la Kenya linasema treni hiyo itapunguza msongamano wa magari barabarani na gharama za usafiri kwa wakazi.
Pia inatarajiwa kuimarisha biashara na uwekezaji katika maeneo yanayopitiwa na reli.
Uzinduzi wa treni hiyo unaashiria mwanzo wa enzi mpya kwa wakazi wa Mombasa, ambapo usafiri wa bei nafuu na wa uhakika sasa unawapa nafasi ya kupanua shughuli zao za kibiashara na kijamii.
Wakaazi wengi waliokusanyika kushuhudia hafla hiyo walieleza matumaini makubwa, wakiona reli hiyo kama kiungo kitakachofungua milango ya uchumi na maendeleo kwa vizazi vijavyo.