Salah akubaliana na Liverpool kuondoka mwishoni mwa msimu wa 2025/26
- Created by Mwandishi Wetu
- Habari
Salah alisema ameamua kuweka wazi mustakabali wake mapema kwa heshima kwa mashabiki.
LIVERPOOL, Uingereza
Mshambuliaji wa Misri Mohamed Salah amekubali rasmi kuondoka katika klabu ya Liverpool FC mwishoni mwa msimu wa 2025/26, akifunga ukurasa wa miaka tisa katika dimba la Anfield.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu, Salah na Liverpool wamefikia makubaliano ya pamoja yatakayomwezesha nyota huyo kumaliza safari yake katika klabu hiyo baada ya msimu huu.
Salah alisema ameamua kuweka wazi mustakabali wake mapema kwa heshima kwa mashabiki.
“Nilitaka mashabiki wajue mapema kwa sababu ya heshima na shukrani zangu kwao,” alisema.
Nyota huyo wa Misri ameandika historia kubwa Liverpool tangu aliposajiliwa kutoka AS Roma mwaka 2017.
Ameisaidia The Reds kushinda mataji makubwa, yakiwemo Ligi Kuu England mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia la Klabu, UEFA Super Cup, FA Cup na Kombe la Ligi mara mbili.
Kwa sasa, Salah amefunga mabao 255 katika mechi 435, akiwa nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Liverpool.
Pia ameshinda kiatu cha dhahabu cha Premier League mara nne, pamoja na tuzo nyingine nyingi binafsi.
Licha ya kuthibitisha kuondoka kwake, Salah amesema bado anaangazia kumaliza msimu huu kwa mafanikio.
Ataaga rasmi mashabiki wa Anfield baadaye mwaka huu baada ya kumalizika kwa kampeni ya 2025/26.
Kuondoka kwake kunatarajiwa kuwa pigo kubwa kwa Liverpool, huku mashabiki wakijiandaa kumuaga mmoja wa wachezaji bora kuwahi kuivaa jezi ya klabu hiyo.