Wasimamizi wadi waonywa dhidi ya kutoa basari kiubaguzi
Gavana wa Kwale Fatuma Achani akihutubia wakazi wa Tiwi katika hafla ya kufungua shule ya chekechea. Picha/Mishi Gongo
Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani amewaonya wasimamizi wa wadi almaarufu watawadi dhidi ya kupeana basari kiubaguzi.
Gavana Achani alisikitika yapo malalamiko kwamba basari zinatolewa kwa misingi ya dini na miegemeo ya kisiasa ya wazazi wa wanufaika.
Alionya serikali itawakabili watakaopatikana na hatia.
Bi Achani aliyekuwa akizungumza katika halfa ya kufungua shule ya chekechea eneo la Tiwi, alisema kuwa kila mtoto wa Kwale ana haki ya kupata ufadhili wa basari bila kufanyiwa ubaguzi.
"Ufadhili wa masomo unaotolewa unapaswa kuwafaidi watoto wote katika Kauti ya Kwale. Ni hatia mtoto kunyimwa ufadhili wa masomo kwa misingi ya kikabili au kidini," Bi Achani alisema.
Gavana huyo aliwahimiza wazazi na wanafunzi kuchukua fomu za basari katika afisi za wadi kaunti nzima ya Kwale ili kunufaika na ufadhili pindi shule zitakapofunguliwa Januari 2025.
Wakati huo huo aliwaonya wazazi ambao wanawahusisha watoto wao na ndoa za mapema na wale wanaowaachilia watoto kuajiriwa.
"Serikali inatoa pesa ili kuwawezesha watoto kutoka familia maskini kupata elimu. Hivyo mzazi atakayekosa kupeleka mwanawe shuleni atachukuliwa hatua,"akasema.
Hadi kufikia sasa Kaunti ya kwale imefadhili zaidi ya wanafunzi 8,000 walio katika shule za upili za kitaifa wanaolipiwa karo kwa asilimia 100.