Mastaa Tanzania waungana na mashabiki kumwomboleza msanii Pembe
Msanii Mzee Pembe ambaye ametagulia mbele ya haki. Picha/Hisani
Mwigizaji wa vichekesho nchini Tanzania Yusuf Kaimu almaarufu kama Pembe, aliyeaga dunia mnamo wikendi, ametajwa kama lejendari ambaye daima mashabiki watamkosa.
Kwa mujibu wa familia, Pembe alikuwa anaumwa na alifariki akiwa hospitalini jijini Dar-es-Salaam kwa matibabu.
Pembe ambaye ni mwigizaji mkongwe wa uchekeshaji, ameacha hofu kwenye tasnia ya sanaa, mastaa maarufu wakikiri kumpoteza mtu muhimu.
Kwenye ukurasa wake, msanii wa filamu nchini humo Jacob Stephen almaarufu kama JB, alimtaja Pembe kama msanii mcheshi na ambaye aliitendea haki nafasi aliyopewa kwenye igizo.
"Daima tutakukumbuka kwa mchango wako kuntu ambao utabaki kama alama kwa wasanii wote nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla wake," aliandika JB.
Kwa upande wake, msanii wa muziki wa kizazi kipya na mkurugenzi wa Crown Media, Ali Kiba almaarufu kama Alikiba, alisema Pembe alikuwa mkarimu, mcheshi na hata mnyenyekevu wakati wote--sio tu 'location' bali hata mtaani.
"Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Tumempoteza lejendari wa uchekeshaji ila kazi ya Mungu haina makosa," aliandika Kiba.
Aidha, wakati wa uhai wake, Pembe alishirikiana na Ulimboka Mwalulesa almaarufu kama Mzee Senga ambaye pia alishtushwa na kifo cha rafiki na msanii mwenzake.
Baadhi ya mashabiki wa Pembe walisema watakosa tabasamu na furaha iliyotokana na muungano wa Pembe na Senga wakidai kwamba walikuwa wameshibana pakubwa katika kufikisha ujumbe.
Kifo chake kilitokea majuma mawili tu baada ya kutokea kifo cha msanii wa miondoko ya Bongo Fleva, Mandojo, ambaye inadaiwa alituhumiwa kuwa mwizi na kuua na umati wenye ghadhabu jijini Dodoma.