Princess Jully wa ‘Dunia Mbaya’ aliimba bila kusoma mistari popote
Marehemu Lilian Auma Aoka almaarufu Princess Jully. Picha/Hisani
Malkia wa muziki wa Benga nchini Kenya, Lilian Auma Aoka almaarufu Princess Jully, aliyeaga dunia Jumamosi alikuwa mkali wa kuimba bila kusoma popote.
Princess Jully aliaga dunia alipokuwa kwa matibabu katika Hospital ya Rufaa ya Migori.
Alikuwa amelazwa kwa zaidi ya muda wa miezi miwili.
Akithibitisha kifo cha msanii huyo, Bw Walter Oguda ambaye ni mwanawe marehemu, alisema Jumamosi kuwa mama yake alikuwa na msukosuko kiafya, hali ambayo imepelekea kuuchukua uhai wake.
"Tumempoteza mtu wa maana sio kwa familia tu bali nchi nzima kutokana na mchango wake katika tasnia ya buradani," alisema Bw Oguda
Wakati wa uhai wake, Princess Jully aling'aa kimuziki ila kubwa zaidi ikawa ni ngoma ya 'Dunia Mbaya' ambayo ilimleta mjini.
Hata hivyo, Princess Jully amekuwa akipambana kutoa ngoma za mafunzo na tahadhari za Ukimwi.
Kulingana na wandani wake, mkali huyo wa Benga, hakuwahi kuingia studio na karatasi wala simu kama wanavyofanya wasanii wengine kusoma huku wakirekodi muziki. Yeye alitiririka mwanzo mwisho.
Kwa sasa mji wa Migori kwenye maeneo ya burudani, muziki wa Princess Jully unapigwa kwa kurudiwarudiwa kama sehemu ya kuenzi mchango wake kwenye tasnia.
"Huyu kazaliwa na kipaji…kuimba kwake ilikuwa ni shauku tu kutoka nafsini. Haijalishi ni wapi, maadamu amealikwa, atafika na kama kawaida atawakilisha mia fil mia," alisema Ronclif Oloo, shabiki wa muziki wa mkali huyo.
Mbali na ‘Dunia Mbaya’ nyimbo zake nyingine ni ‘Amayo Charles’, ‘Yuko Wapi’, na ‘Min Caro’ miongoni mwa nyingi nyingine.