Kocha Pep Guardiola wa Man City alia kuingia fainali ya Carabao na Arsenal
- Created by Mwandishi wa AVDelta
- Habari
Kwa fikira za Guardiola, hata kama alikuwa akifanya mzaha, fainali ya Carabao inafaa kuwa uwanja usio wa timu yoyote.
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amewafurahisha mashabiki wa Arsenal kwa kutoa kauli inayoonyesha kuiogopa timu hiyo.
Guardiola ambaye timu yake iliwazamisha vijana wa kocha Eddie Howe kwa 3-1 (jumla 5-1), alianza malalamishi punde tu baada ya kipenga cha mwisho uwanjani Etihad.
Badala ya kufurahia kuingia fainali ya kombe la Carabao, Mhispania huyo anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu alianza visingizio.
“Tunaenda London Kaskazini. Wao Arsenal watatusubiri huko. Sisi kila wakati tunasafiri. Hakuna yeyote anayeenda kaskazini mwa England kwa fainali,” Guardiola alisema.
Kawaida fainali za mashindano yote Uingereza huchezwa katika uwanja wa Wembley, ambao uko Kaskazini mwa jiji la London sawa na ule wa Emirates. Wembley Stadium iko karibu kilomita kumi kutoka Emirates Stadium.
Kwa fikira za Guardiola, hata kama alikuwa akifanya mzaha, fainali ya Carabao inafaa kuwa uwanja usio wa timu yoyote. Lakini Arsenal watakuwa tu kwao nyumbani.
Jiji la Manchester liko kaskazini mwa Uingereza, kilomita kama 350 kutoka uwanja wa Wembley.
Kocha huyo pia alionyesha kukerwa kwake kuhusu Marc Guehi kutoruhusiwa kucheza fainali. Alisema haelewi kwa nini mchezaji aliyejiunga Januari hawezi kuhusika kwenye fainali hiyo.
“Unanunua mchezaji kwa pesa nyingi, ilhali hawezi kucheza kwa sababu ya sheria ambayo sielewi,” alisema.
Kocha huyo alisema Manchester City watatuma rufaa kwa Shirikisho la Soka Uingereza (Football Association- FA).
"Tutawaomba waangalie upya hizi kanuni," akasema.
Fainali ya Carabao imepangwa kuwa Machi 22, ambapo Guardiola atakutana kwa mara ya kwanza na aliyekuwa msaidizi wake, Mikel Arteta kwenye fainali yoyote.