Utajiju! EFL yamwambia Guardiola kuhusu Marc Guehi
- Created by Juma Namlola
- Habari
Kanuni za EFL zinasema wazi kwamba mchezaji hatahifadhiwa kucheza kwenye fainali ikiwa alisajiliwa kwa timu yake mpya baada ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali.
Wasimamizi wa masindano ya mpira Uingereza, English Football League (EFL) wamejitokeza kujibu matamshi ya kocha wa Manchester City Pep Guardiola kuhusu sajili mpya Marc Guehi.
Guardiola alilalama usiku wa Jumatano kwamba ni maonevu kwa timu yake kumwaga mihela kumnasa beki Guehi na kuishia kwamba hataruhusiwa kucheza fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Arsenal.
Guardiola aliibua suala hilo baada ya City kufuzu fainali kwa jumla ya mabao 5–1 dhidi ya Newcastle United.
Alieleza kwamba ni vigumu kuelewa kwa nini Guehi, ambaye ni mchezaji wa City na analipwa mshahara na klabu hiyo, hawezi kucheza.
Hata hivyo, kanuni za EFL zinasema wazi kwamba mchezaji hatahifadhiwa kucheza kwenye fainali ikiwa alisajiliwa kwa timu yake mpya baada ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali.
Guehi, alijiunga na City kutoka Crystal Palace Januari 19, baada ya mchezo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya Newcastle.
"EFL haitabadilisha kanuni zake ili kumruhusu mchezaji kucheza fainali ya Machi 22, 2026. Kanuni hizi ziko wazi na zimetekelezwa kwa miaka sasa," ilisema taarifa ya EFL.
Shirikisho hilo lilisema kama lingekuwa halitaki wachezaji wapya, basi hata Antoine Semenyo asingecheza.
Lakini raia huyo wa Ghana alijiunga na City kabla ya mchezo wa kwanza wa nusu fainali. Aliruhusiwa kucheza na atacheza fainali uwanjani Wembley.
Haijaeleweka sababu za wasiwasi wa Guardiola, ikizingatiwa kuwa Manchester City iko na mabeki wengi wenye uzofu wa kupambana na washambuliaji wa Arsenal.